Ruto: Ningependa kukutana na vijana kusikiliza maoni yao

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amependekeza mkutano kati yake na vijana wa taifa hili ambao walikuwa mstari wa mbele kupinga mswada wa fedha ili kusikiliza maoni yao.

Akizungumza katika ikulu ya Nairobi wakati wa kutangaza uamuzi wake wa kutotia saini mswada wa fedha wa mwaka 2024, Rais alisema pia kwamba mkutano huo utatoa fursa ya kujadili sehemu ambazo zinafaa kupatiwa kipaumbele.

“Ninapendekeza kwamba katika muda wa siku 14 zijazo, mkutano wa wadau wa sekta mbali mbali uandaliwe ili kujadili namna ya kushughulikia masuala yaliyo kwenye mswada huu.” alisema Rais Ruto.

Aliongeza pia kwamba watajadili mikakati ya kuboresha vita dhidi ya ufisadi humu nchini.

Linalosubiriwa sasa ni kuona jinsi mkutano huo utaandaliwa ikitizamiwa kwamba vijana walioongoza maandamano almaarufu Gen Z wamekuwa wakisisitiza mitandaoni kwamba hawana viongozi ambao wamewachagua na kwamba kila mmoja amekuwa akijiongoza wakiwa na dhamira sawa.

Huku hayo yakijiri, Rais alitoa risala za rambirambi kwa familia ambazo wanao walifariki wakati wa maandamano hiyo jana.

Website |  + posts
Share This Article