Hali itakuwa ngumu kabla ya kuwa bora, aonya Ruto

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto amesema atafanya maamuzi sahihi kwa niaba ya nchi hii. 

Amesema serikali inaangazia manufaa ya muda mrefu ambayo hatimaye yatawafaidi Wakenya.

“Hatupaswi kuangazia manufaa ya muda mfupi katika mitazamo yetu katika kushughulikia masuala mbalimbali,” alisema Rais Ruto.

Alisema hatachukua njia rahisi na maarufu bali ile muhimu, jasiri na yenye kuleta mabadiliko.

Alikiri kuwa njia hii itafanya hali kuwa ngumu, lakini “hii itafanya nchi yetu kubadilika milele”.

Ruto aliyasema hayo leo Alhamisi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa viongozi wakuu wa serikali ya kitaifa unaofanyika mtaani South C, Nairobi.

Mkutano huo unahudhuriwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Mawaziri, Makatibu na maafisa wengine waandamizi serikalini.

Rais aliuambia mkutano huo kwamba kusudi lake sio kushinda uchaguzi bali kubadilisha nchi hii kwa manufaa ya raia wake.

“Lengo langu ni kuibadilisha Kenya na kufanya vizazi vijavyo kustawi.”

Aliongeza kuwa Kenya inaelekea kujitosheleza kichakula kutokana na mpango wa serikali wa kutoa ruzuku kwa uzalishaji wa chakula.

“Sasa tuko na dhamira ya kubuni nafasi za ajira na kulipa madeni yetu. Kenya haitashindwa kulipa madeni yake.”

Alitetea ziara zake za hivi karibuni nje ya nchi akisema zinailetea nchi hii manufaa mengi.

“Tumeinadi mno Kenya; sasa ni nchi inayopendwa na wawekezaji na watalii wengi.”

Rais aliongeza kuwa Kenya ina uhusiano thabiti na washirika wake wa kimaendeleo.

“Tumepandisha hadhi yetu duniani.”

Kwa upande wake, Gachagua alielezea kuwa mikutano ya mara kwa mara inatoa fursa kwa serikali kutathmini ilichofanya.

“Tuna kandarasi na watu wa Kenya ambayo inaweza tu kutolewa upya kutokana na utendakazi wetu wenye mafanikio,” alisema Naibu Rais.

Share This Article