Taarifa ya PCS
Rais William Ruto amezindua mikataba 20 ya uwekezaji yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 2.9 ambayo itabuni nafasi bora 63,000 za ajira kwa Wakenya.
Mikataba hiyo inahusisha nyanja za kilimo, uzalishaji, ICT, afya, nishati, mali isiyohamishika na kadhalika.
Rais Ruto amesema mingi ya mikataba hiyo inakaribia kutekelezwa, huku mingine kadhaa tayari ikiwa inatekelezwa.
Alielezea kuwa uwekezaji huo ni ishara ya imani ya wawekezaji nchini Kenya.
“Hatuzungumzii tu idadi; tunazungumzia uwekezaji halisi, ikiwa ni pamoja na dola bilioni moja katika kilimo pekee,” alisema Ruto.
Aliyasema hayo wakati wa Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kenya lililoandaliwa jijini Nairobi leo Jumatano.
Rais wa Msumbiji Daniel Chapo ambaye anafanya ziara ya siku tatu nchini ni miongoni mwa waliohudhuria.
Ruto akitumia fursa hiyo kusema serikali daima inatekeleza mageuzi makubwa kwa kusudi la kuimarisha ushindani wa uwekezaji nchini, kurahisisha mazingira ya kufanya kazi na kubuni mazingira bora ya uwekezaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi alisema usumbufu wa kimataifa kama vile mgogoro wa Iran, ambao umevuruga usafirishaji duniani, ni sababu tosha ya kuwepo ushirikiano ulioboreshwa baina ya mataifa ya Afrika, ili kupunguza changamoto kutoka nje.
Waziri wa Uwekezaji na Biashara Lee Kinyanjui alisema wizara yake inafanya kazi na wawekezaji na kushughulikia mahitaji yao.