Ruto asema atakuwa mhubiri baada ya kustaafu

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amesema kwamba mpango alionao baada ya kustaafu ni kurejelea mwito wake asilia ambao ni kuhubiri.

Akizungumza wakati wa ibada ya jana Jumapili huko Bungoma, kiongozi wa nchi alitetea tabia yake ya kuzungumza kwenye madhabahu na kuhutubia wananchi juu ya magari akisema inatkana na mwito huo.

Wakati huo huo Rais aliwataka viongozi wa dini kuendelea kuombea taifa hili anapojizatiti kufufua uchumi na kulainisha sehemu mbali mbali katika utawala wake.

Alisema nchi iko katika mwelekeo sawa wa kuafikia ukuaji akisema miito ya utawala bora imechochea haja ya uwajibikaji wa pamoja na uadilifu.

Kulingana naye, Mungu ameipa Kenya hali nzuri ya anga kwa miaka miwili iliyopita na sasa kuna chakula cha kutosha nchini huku maongezi kuhusu maendeleo yakibadilika pakubwa.

Wanaopania kueneza ukabila na migawanyiko walionywa na Rais Ruto aliyesema ataongoza miito ya umoja nchini kazi aliyoanza kwa kuunda serikali jumuishi.

Baadaye jana kiongozi wa nchi aliondoka Kenya kuelekea jijini Beijing nchini China ambapo atahudhuria kongamano la ushirikiano wa China na mataifa ya bara Afrika.

Share This Article