Ruto aongoza kikao cha dharura cha EAC kujadili DRC

Viongozi walitaka kundi la M23 kusitisha mapigano ili kutoa fursa kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu mjini Goma.

Dismas Otuke
2 Min Read

Rais William Ruto, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), jana aliandaa kongamano la 24 lisilo la kawaida na viongozi kadhaa kupitia mtandao kujadili hali ya kiusalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kikao hicho kilifahimishwa hali ilivyo mjini Goma mashariki mwa DRC huku viongozi wakikuhimiza haja ya hatua za dharura kuchukuliwa ili kurejesha utulivu.

Baadhi ya mapendekezo ya kikao hicho ni pamoja na serikali ya DRC  kutoa ulinzi kuzuia mashambulizi ya balozi za kigeni nchini humo na raia wa kigeni.

Aidha viongozi walitaka kundi la M23 kusitisha mapigano ili kutoa fursa kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu mjini Goma, kuandaliwa kwa mazungumzo ya maridhiano kati ya serikali ya Congo, kundi la M23, waasi wengine walio na silaha, na wadau wote ili kutafuta suluhu ya kudumu.

Viongozi hao walitoa rambirambi zao kwa waliofariki na familia zilizopoteza jamaa zao kutokana na mapigano hayo.

Vilevile, kikao hicho kilimjukumisha Ruto kufanya kikao na mwenyekiti wa shirika la maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), ambao pia wanaongoza juhudi za upatanisho ili kuwa na mtazamo mmoja.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda, William Ruto wa Kenya, Evariste Ndayishimiye wa Burundi, Samia Suluhu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Yoweri Museveni wa Uganda, Hassan Sheikh Mahammud wa Jamhuri ya Somalia, na Salvar Kiir wa Sudan Kusini.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *