Ruto ahimiza nchi za Afrika kuimarisha biashara kati yao

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ametoa wito kwa nchi za bara la Afrika kufanya biashara zaidi miongoni mwao, akiitaja hiyo kuwa silaha bora zaidi ya kuangamiza umaskini barani humo.

Ruto amesikitika kuwa nchi za bara la Afrika zinaendelea kufanya biashara zaidi na nchi zilizo nje ya bara hilo, mwenendo ambao alisema unapaswa kubadilishwa.

Ameongeza kuwa biashara kati ya nchi za Afrika ni ya kiwango cha chini cha asilimia 15 ya jumla ya biashara barani humo ikilinganishwa na asilimia 60 barani Ulaya na Asia.

“Ili bara letu la liweze kufikia uwezo wake mkubwa, kubuni fursa na utajiri kwa ajili ya raia, na kufikia ustawi jumuishi, Afrika lazima ifanye biashara zaidi na yenyewe,” alisema Ruto.

Hata hivyo, aliongeza kuwa Afrika inachukua hatua za kuboresha biashara kati ya nchi za bara hilo, hasa kutokana na kutekelezwa kwa makubaliano ya Biashara Huru barani Afrika (AfCTA).

“Inakadriwa kuwa biashara kati ya nchi za Afrika inaweza kuongezeka kwa kiwango kikubwa hadi asilimia 50 kufikia mwaka 2035, na kubuni utajiri mkubwa, kubuni mamilioni ya nafasi za ajira, kuongeza fursa za biashara ndogo na kufungua masoko ya bidhaa na huduma kutoka barani humo,” alisema Rais.

Ili hili kutimia, kiongozi wa nchi alisema Afrika lazima ikifanyie mabadiliko na kufufua kilimo, kuufanyia mabadiliko mfumo wa kutoa mikopo duniani mbali na kuanzisha mfumo wake, na kutoa jukwaa la sekta binafsi kutekeleza wajibu wa kuchochea maendeleo.

Ruto aliyasema hayo kwenye Nguzo ya Kiuchumi ya Biashara na Uwekezaji katika Mkutano wa Kimataifa wa 9 wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 9) jijini Yokohama nchini Japani.

Mkutano huo uliingia siku ya pili leo Alhamisi.

Website |  + posts
Share This Article