Ruth Matete ashauri watu kuangazia ukuaji wa kibinafsi

Marion Bosire
1 Min Read

Mwimbaji wa nyimbo za injili, Ruth Matete ambaye pia ni mhubiri ametoa ushauri kupitia mitandao ya kijamii kwa wafuasi wake kuhusu umuhimu wa kuangazia ukuaji wa kibinafsi.

Matete kupitia akaunti yake ya Instagram alisema kwamba kila mmoja kwenye mitandao ya kijamii hudhania kwamba maisha ya wengine ni bora kuliko yake, kauli ambayo huenda ikawa kweli au uongo.

Kulingana naye, wanaoonekana kuwa sawa wametia bidii au kukosa kwa watu kutia bidii kunawafanya wadhanie kwamba wengine wako sawa zaidi yao.

Anasema mapambano ya maisha husababisha kulinganisha maisha na wivu na anashauri kila mmoja kuangazia safari yake ya maisha.

Mama huyo wa mtoto mmoja ambaye sasa anaishi nchini Canada alisisitiza kwamba hatua ya kuangazia maisha ya wengine humfanya mtu kusahau maisha yake.

“Ni muhimu kuelewa kwamba hakuna mtu anakuja kukuokoa. Lazima uwe bingwa wako binafsi, ukiangazia matarajio yako na ndoto zako.” alisema Ruth.

Himizo lake kwa wafuasi wake ni kwamba wasiangazie walio kinyume nao bali waangazie bidii na kujitolea katika kutafuta kuboresha maisha yao.

“Watu huwa hawatangazi mapungufu yao. Wanaangazia ukuaji na hatua hiyo husababisha mfananisho usio sawa.” Alisema mwimbaji huyo.

Share This Article