Ruger azuka na mwonekano mpya

Msanii huyo yuko likizoni jijini Paris nchini Ufaransa na alichapisha mitandaoni picha za mwonekano huo mpya.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Nigeria Ruger ambaye jina lake halisi ni Michael Adebayo Olayinka, ameshangaza mashabiki wake na mwonekano mpya ambao umesababisha minong’ono.

Ruger ambaye wengi wanamfahamu kwa mwonekano wake wa nywele iliyopakwa rangi ya waridi na jicho moja lililofunikwa, sasa amekumbatia mwonekano ambao wengi wameutaja kuwa wa utu uzima.

Amenyoa nywele kabisa, ameongeza chuma kwenye meno na badala ya kufunika jicho moja sasa anavaa miwani ya rangi nyeusi.

Chapisho la msanii huyo kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii lilikuwa fupi lakini limevutia hisia mseto kutoka kwa mashabiki wake.

Alichapisha picha kadhaa na kuandika, “Segun likizoni Paris”.

Huku wengine wakililia mwonekano wake wa zamani, wengine wanafurahia mwonekano wake mpya wakimtania kwamba sasa hata mamake mzazi amefurahi ikitizamiwa kwamba wazazi wengi wa kiafrika hawapendelei wanao kuwa na rangi tofauti na nyeusi kichwani.

Jamaa kwa jina Ini Cash aliandika, “Najua mama anafurahia sana sasa”. Zayinarb aliandika, “Iko wapi nywele yako ya waridi?” huku mwingine kwa jina Mc Lioon1 akimtania kwamba kichwa chake ambacho amenyoa kipara ni kizuri kugonga gonga.

Lakini wapo wengine pia wanaamini kwamba msanii huyo ametumia uwezo wa akili mnemba kubadili picha zake kuhadaa mashabiki na wanasema wataamini mwonekano mpya watakapomtia machoni.

Share This Article