Ripoti: Helikopta iliyomuua Jenerali Ogolla ilianguka kufuatia hitilafu ya injini

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akikabidhiwa ripoti ya kilichosababisha ajali ya helikopta iliyomuua marehemu Francis Ogolla

Rais William Ruto amekabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa kilichosababisha kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi nchini, KDF Francis Ogolla. 

Ogolla, aliyekuwa na umri wa miaka 61, alifariki akiwa na maafisa wengine tisa huku maafisa wengine wawili wa kijeshi wakinusurika ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea Aprili 18, 2024 katika eneo la Sindar kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Marehemu Ogolla alikuwa akiongoza misheni ya kurejesha amani katika eneo linalokabiliwa na changamoto ya wizi wa mifugo la Pokot Magharibi wakati ajali hiyo ilipotokea.

Kulingana na ripoti hiyo, ushahidi uliokusanywa unaashiria helikopta hiyo ilianguka  kutokana na hitilafu ya injini.

Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya alimkabidhi Rais Ruto ripoti ya uchunguzi wa ajali hiyo katika Ikulu ya Nairobi leo Ijumaa.

Alikuwa ameandamana na maafisa wa ngazi ya juu jeshini wakati wa ukabidhi wa ripoti hiyo.

Maafisa wengine waliofariki wakati wa ajali hiyo ni pamoja na:

1. Brigedia Swale Saidi,
2. Kanali Duncan Keittany,
3. Luteni Kanali David Sawe,
4. Meja George Benson Magondu,
5. Kapteni Sora Mohamed,
6. Kapteni Hillary Litali,
7. Sajini Mwandamizi John Kinyua Mureithi,
8. Sajini Cliphonce Omondi, na
9. Sajini Rose Nyawira.

Jenerali Ogolla ambaye alikuwa katika helikopta aina ya Huey, alikuwa ameondoka jijini Nairobi Aprili 18 asubuhi kuwatembelea wanajeshi ambao wanahudumu eneo la North Rift chini ya operesheni ya Maliza Uhalifu, pamoja na kukagua shughuli za ukarabati wa shule katika eneo hilo.

Kufuatia kifo cha Ogolla, Rais Ruto alitangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa, huku bendera ya taifa, ya jeshi na ile ya Afrika Mashariki zikipeperushwe nusu mlingoti kuanzia  Aprili, 19, 2024

Website |  + posts
Share This Article