Mwili wa mwanamuziki Rigobert Bamundele, maarufu kama Rigo Star umezikwa jijini Paris nchini Ufaransa.
Rigo ambaye aliangazia sana uchezaji gitaa alikata roho usiku wa Oktoba 25 nchini Ufaransa na alizikwa Jumanne, Novemba 21, 2023 nchini humo.
Hafla ya mazishi ya kidini iliandaliwa katika eneo moja la makaburi jijini Paris ambako gwiji huyo wa kupiga gitaa wa asili ya Congo alipumzishwa.
Wengi wa wanamuziki wenza kutoka Congo ambao wanaishi Ufaransa walihudhuria hafla ya mazishi ya Rigo Star.
Rigo alikuwa maarufu sana katika ulingo wa muziki wa Congo miaka ya 1970 hadi 1990, ambapo alifanya kazi na bendi ya Viva la Musica iliyokuwa ikiongozwa na marehemu Papa Wemba na mwimbwaji wa kike M’Bilia Bel.
Alifariki akiwa na umri wa miaka 68 na katika miaka yake ya mwisho mwisho, alikuwa ameacha kujihusisha na muziki kutokana na matatizo ya kiafya.
Awali, ilidhaniwa kwamba mwili wake ungesafirishwa hadi nchini Congo kwa mazishi.