Ray C aomba maoni ya mashabiki kuhusu kurejelea muziki

Amesema anatamani kurejelea muziki kabisa nchini Tanzania.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Rehema Chalamila maarufu kama Ray C, ameomba mashabiki zake maoni kuhusu kurejelea muziki nchini Tanzania.

Kupitia akaunti yake Instagram Ray C alichapisha video ya mwanamuziki wa kike jukwaani na kuandika, “Kila nikimuangalia huyu Binti najiona, halafu najimiss, halafu namiss pia steji, halafu namiss pia mashabiki,”.

Aliendelea kuelezea jinsi anatamani kurejea kufanya kazi na waandaaji muziki wa nyumbani Tanzania huku akiuliza mashabiki, ” Je naomba kuwauliza !!!! Kweli mna Kiu na Ray C arudi nyumbani kwenye game rasmi ?????”.

Ray C aliwataka kuweka mawazo yao chini ya chapisho lake ambapo wengi akiwemo mwigizaji wa Tanzania Lissah aliyeandika, “Tunakukosa sana!”

Sharifa3728 aliandika, “Sijuwi kwanini umepiga kimyaaa mtu wangu”, Straightfoward_Rae akaandika, “Rudi kwenye muziki, ni kitu unachokipenda” huku Nkubitu akiandika, “Mimi ni Mkenya na nitasema rudi kwenye kitu ambacho unakipenda,”.

Mwimbaji huyo ambaye ni mmoja wa walioanzisha muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania amesalia kimya kwa muda hasa baada yake kuhamia nchini Ufaransa ambako alijaliwa mtoto mmoja.

Hata hivyo amekuwa akitoa nyimbo moja moja huku akigusia kuhusu kurejea nchini Tanzania ili kuwapa watu wake wa nyumbani muziki waupendao.

Ray C wa umri wa miaka 44 sasa mzaliwa wa Iringa nchini Tanzania, alianza rasmi muziki mwaka 2001 na kufikia 2003 akazindua albamu yake ya kwanza kwa jina “Mapenzi Yangu”.

Ana albamu nyingine tatu ambazo ni ‘Na Wewe Milele; ya mwaka 2004, ‘Sogea Sogea’ ya mwaka 2006 na ‘Touch Me’ ya mwaka 2008.

Share This Article