Rais William Ruto azindua kituo kidogo cha umeme Athi River

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amezindua kituo cha kuzalisha umeme huko Athi River, kaunti ya Machakos. Alizindua kituo hicho jana Jumanne katika kaunti ndogo ya Mavoko.

Kituo hicho ni mojawapo ya vituo vidogo vya kuzalisha umeme kiwango cha kilo volt 220 katika eneo la Nairobi na ni mradi wa ruwaza ya mwaka 2030.

Rais Ruto alisema kituo hicho kitasaidia sana kukabiliana na tatizo la kukatika kwa umeme kila mara.

Akizungumza na wananchi muda mfupi baada ya kuzindua kituo hicho, Ruto alisema kwamba serikali yake iliamua kuongeza kituo hicho cha kuzalisha umeme ili iweze kupanua ukanda maalum wa kiuchumi wa Athi River.

Alisema ukanda huo umetoa ajira kwa vijana wapatao elfu 20 na wangependa kuongeza vijana wengine elfu 15 huko na kwamba wametenga shilingi bilioni moja kwa upanuzi wa ukanda huo kwani wanaendelea kujadiliana na Amerika kuhusu sheria ya ukuaji na fursa barani Afrika.

Sheria hiyo alisema inatoa fursa ya kuuza bidhaa zilizoundwa nchini Kenya huko Amerika.

Ruto alihimiza vijana wajipange kwani amepiga marufuku ununuzi kutoka nchi za nje bidhaa kama vile samani ambazo zinaweza kuundwa humu nchini.

Alitumia fursa hiyo kuonya uongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya dhidi ya kuandaa maandamano leo Jumatano akisema serikali yake haitatizama tu waandamanaji wakiharibu mali ya Wakenya wengine na baadhi yao wakipoteza maisha kwa sababu ya maandamano jinsi ilivyokuwa wiki jana.

Website |  + posts
Share This Article