Tamasha ya muziki yaahirishwa Nyanza kwa sababu ya maandamano

Martin Mwanje
2 Min Read
Picha imepigwa na KNA
Tamasha ya muziki ya siku nne iliyoleta pamoja shule zote katika eneo la Nyanza na kuandaliwa katika kaunti ya Migori imeahirishwa.
Hii ni kufuatia maandamo yaliyoratibiwa kufanyika leo Jumatano kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya juu maisha na kubatilisha sheria ya fedha ya mwaka 2023.
Akithibitisha kuahirishwa kwa tamasha hiyo, kamishna wa kaunti ya Migori David Gitonga alielezea hofu ya usalama kwa wanafunzi kutokana na maandamano hayo kuwa sababu ya kuchukuliwa kwa hatua hiyo.
Tamasha ya muziki iling’oa nanga Jumatatu wiki hii na ilitarajiwa kumalizika kesho Alhamisi.
Tamasha hiyo liliwaleta pamoja zaidi ya wanafunzi 13,000 ambao wanashindana katika vitengo mbalimbali kuanzia shule ya chekechea hadi kidato cha nne.
Kuahirishwa kwa tamasha hiyo kunakuja wakati ambapo wafanyabiashara wengi katika miji ya Nairobi, Kisumu na Kisii miongoni mwa maeneo mengine waliamua kufunga biashara kwa hofu ya mali yao kuporwa na waandamanaji.
Maafisa wa usalama pia wameripotiwa kurusha gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika eneo la Mathare mjini Nairobi, na katika miji ya Mombasa na Migori ili kuwatawanya waandamanaji.
Serikali imeonya kukabiliana vikali na mtu yeyote atakayepatikana akijihusisha katika visa vya uvunjaji wa sheria ikiwa ni pamoja na uporaji na uharibifu wa mali.
Maandamano ya leo Jumatano yameitishwa na muungano wa Azimio kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya juu ya maisha.
Watu sita walifariki wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na muungano huo Jumatano wiki iliyopita na Rais William Ruto ametoa onyo kali akisema serikali yake haitakubali kutokea kwa maafa ya Wakenya kwa sababu ya maandamano.
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *