Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump kutofika mahakamani

Marion Bosire
1 Min Read
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump

Aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump ameamua kutofika mahakamani kutoa ushahidi kwa mara ya pili kwenye kesi ya ulaghai dhidi yake huko New York.

Trump anasema hana lolote la kuongeza.

Alisema Jumapili kwamba haoni haja ya kutoa ushahidi kwani alifanya hivyo kwa njia iliyofanikiwa na kamilifu mwezi jana.

Trump ambaye anapendelewa sana kwenye uteuzi wa mgombea urais katika chama cha Republican, alikuwa anatarajiwa kurejea mahakamani Jumatatu Disemba, 11, 2023.

Katika kesi hiyo, Trump, watu wa familia yake na wafanyakazi wake wanatuhumiwa kwa kuongeza maradufu thamani ya mali yake kwa nia ya kupata mikopo mikubwa kutoka benki na masharti nafuu ya bima.

Wakili wake kwa jina Christopher Kise naye ameunga mkono maneno ya mteja wake akisema hakuna cha kuongeza mbele ya jaji ambaye amewawekea amri iliyo kinyume cha sheria na ambaye anaonekana kama ambaye alipuuza ushahidi wa Trump na wa wahusika wengine.

Mwanasheria mkuu wa New York Letitia James, ambaye aliwasilisha kesi hiyo mahakamani, alisema kwamba afisi yake tayari imethibitisha kwamba Trump alitekeleza makosa ya kifedha kwa miaka mingi na kujitajirisha kwa njia isiyofaa.

Share This Article