Rais wa Msumbiji Daniel Francisco Chapo ameanza ziara rasmi ya siku tatu nchini Kenya kwa lengo la kuimarisha ushirikiano, kupanua biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Rais Chapo aliwasili nchini Kenya jana Jumanne kwa mwaliko wa Rais William Ruto.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Chapo alilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi.
Mudavadi alitaja ziara hiyo kuwa fursa muhimu kwa nchi hizo mbili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama.
Alidokeza kuwa mashauriano na Rais huyo yatahusu kuboreshwa kwa ushirikiano kati ya Kenya na Msumbiji.
“Ziara hii itatoa fursa bora kwa Marais hao wawili kukadiria hali ya sasa ya ushirikiano wa kidiplomasia pamoja na kubadilishana mawazo kuhusu maswala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, usalama na amani katika nchi hizi mbili,” alisema Mudavadi.
Wakati wa ziara yake nchini, Rais Chapo anatarajiwa kuhudhuria Kongamano la 4 la Kimataifa kuhusu Uwekezaji litakaloandaliwa katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC.