Rais Vladimir Putin kukosa mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Urusi Vladimir Putin hatahudhuria mkutano wa nchi za BRICS ambazo ni Brazil, Urusi, India na China utakaoandaliwa nchini Afrika Kusini Agosti, 2023, baada ya makubaliano ya pande zote. Hii ni kwa mujibu wa Rrais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.

Kwenye taarifa, msemaji wa Rais Ramaphosa Vincent Magwenya alielezea kwamba Urusi itawakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov kwenye mkutano huo.

Taifa la Afrika Kusini lilijipata kwenye njia panda kuhusu kuandaa mkutano huo kwa sababu ni mwanachama wa mahakama ya kimataifa ya jinai, ICC ambayo imetoa kibali cha kumkamata Putin tangu mwezi Machi. Kutokana na hilo, Afrika Kusini inajukumiwa kumtia mbaroni Putin iwapo ataingia nchini humo.

Suala hilo limesababisha mjadala mkubwa nchini Afrika Kusini na nchi za magharibi kuhusu iwapo nchi hiyo inafaa kutekeleza hitaji la kumkamata kiongozi huyo. Afrika Kusini ilitangaza kwamba haiungi mkono upande wowote katika vita kati ya Ukraine na Urusi ambavyo ndio sababu kuu ya Putin kushtakiwa ICC.

Afrika Kusini ina uhusiano mwema pia na Urusi.

Mwaka 2015, Afrika Kusini ilijipata katika hali sawia ambapo Rais wa Sudan wakati huo Omar Al-Bashir aliizuru huku kukiwa na kibali cha kumkamata kutoka mahakama ya ICC. Bashir hata hivyo hakukamatwa.

Viongozi wa nchi nyingine za kundi hilo ambazo ni Brazil, India na Afrika Kusini watahudhuria mkutano huo wa Agosti.

Kundi la BRICS ambalo ni la uwezo wa kiuchumi, lilianzishwa mwaka 2019 na wakati huo lilikuwa na nchi za Brazil, Urusi, India na China yaani BRIC na baadaye Afrika Kusini ikajiunga nalo ndio likawa BRICS.

Nchi nyingine kama Ethiopia, Iran na Argentina zimetuma maombi ya kujiunga na kundi hilo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *