Rais wa Tanzania Samia Suluhu ametuma risala za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao katika ajali ya basi iliyotokea katika eneo la Mtama mkoani Lindi.
Watu 15 walifariki wakati wa ajali hiyo iliyotokea baada ya basi hilo kukumbwa na hitilafu za breki.
“Nawapa pole wafiwa waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ya basi iliyotokea eneo la Mtama mkoani Lindi na kusababisha vifo vya watu 15. Mwenyezi Mungu awe faraja kwetu sote, awarehemu ndugu zetu hawa waliotutoka na kuwajalia majeruhi pona ya haraka,” Rais Suluhu alisema katika rambirambi zake.
“Tunapoelekea msimu wa mwisho wa mwaka, naviagiza vyombo vya ulinzi na usalama barabarani kuongeza usimamizi wa sheria na ukaguzi.”
Visa vya kutokea kwa ajali barabarani hukithiri hasa wakati wa msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya katika nchi za Afrika Mashariki huku wahudumu wa magari wakiwa mbioni kujipatia faida kubwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wasafiri.
Mara nyingi, maonyo ya serikali kuwa watakaokiuka sheria za barabarani watachukuliwa hatua kali hutua kwa sikio la kufa.
Haijulikani ikiwa onyo la Rais Suluhu litazingatiwa wakati huu.