Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kwamba anaamini katika uhuru wa wanahabari na wala sio katika kuhujumu uhuru huo akiongeza kwamba vyombo vya habari sio mshindani wa serikali.
Akizungumza wakati wa kongamano la kutathmini maendeleo ya sekta ya habari nchini Tanzania lililoandaliwa katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema kwamba vyombo vya habari ni mshirika muhimu wa serikali.
Rais huyo alikumbusha wanaohudhuria kongamano hilo kwamba aliwahi kuandaa kikao na wahariri wa vyombo vya habari ili kubadilishana mawazo, siku chache baada ya kuapishwa kuwa rais wa nchi hiyo.
Wakati huo aliwahakikishia ushirikiano mkubwa na kuahidi kulinda uhuru wa Vyombo vya habari.
Kiongozi huyo aliridhika kwamba malalamiko kuhusu uhuru wa vyombo vya habari yamepungua akisema vyombo vya habari vinasaidia kujuza, kuelimisha na kuburudisha wasikilizaji na watazamaji katika kila pembe ya nchi ya Tanzania.
Alikiri kwamba awali kulikuwa na mvutano kati ya viongozi serikalini na vyombo vya habari lakini wakaona kwamba hatua hiyo haikuwa na manufaa ya aina yoyote.
“katika kipindi hicho hatukufika sehemu nzuri lakini tulipoamua kukaa pamoja tunaona.” alisema Rais Samia akimalizia kwamba serikali haina budi ila kuweka mifumo ya kisera, kisheria na Kitaasisi katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari.