Inspekta Jenerali wa polisi akutana na polisi wa Haiti

Marion Bosire
2 Min Read

Inspekta jenerali wa polisi Japhet Koome leo alifanya mkutano na ujumbe wa polisi wa taifa la Haiti katika afisi yake jijini Nairobi.

Mkutano huo uliohudhuriwa pia na manaibu wa Koome, Douglas Kanja na Noor Gabow unajiri wakati ambapo Kenya inajiandaa kutuma maafisa wa polisi nchini haiti kusaidia kurejesha amani.

Joachim Prohete mmoja wa wasimamizi wa polisi nchini Haiti alisema kwamba wanategemea sana usaidizi wa Kenya ili kuhakikisha usalama wa watu wa Haiti.

Haiti iliitisha usaidizi wa kimataifa katika kukabiliana na magenge yaliyojihami yanayotatiza amani nchini humo hatua iliyochochea baraza la usalama la umoja wa mataifa kuchukua hatua.

Kenya iliridhia kutuma maafisa wake wa polisi wapatao elfu moja nchini Haiti kuongoza oparesheni ya kurejesha amani nchini humo. Kundi la kwanza la maafisa hao wa Kenya lilistahili kufika Haiti mwezi Mei mwaka huu wa 2024.

Mpango huo hata hivyo ulisimamishwa ili kutoa fursa kwa kuundwa kwa serikali mpya nchini Haiti kulingana na matakwa ya makundi hayo yaliyojihami.

Wawakilishi wa makundi hayo ya waasi walimtaka waziri mkuu wa Haiti wakati huo Ariel Henry ajiuzulu kabla ya kuruhusiwa kurejea nchini humo kutoka Kenya ambako alikuwa amefanya ziara rasmi.

Serikali mpya ya Haiti ilibuniwa mwezi huu ambapo maafisa wa ngazi mbali mbali walichaguliwa kuchukua mahala pa waliokuwa wakihudumu chini ya Ariel Henry.

Baraza la mpito lilimteua Garry Conille kuwa waziri mkuu.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *