Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefafanua kuhusu tuzo aliyopokea jana ya ‘The Global Goalkeeper’ ambayo hutolewa na wakfu wa Bill and Melinda Gates.
Kiongozi huyo amesema tuzo hiyo ni thibitisho kwamba dunia imetambua juhudi za Tanzania katika kuboresha huduma za afya, hususan kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Rais Samia amesema serikali imeweka mipango madhubuti na kuongeza jitihada zaidi ili kuhakikisha kwamba kufikia mwaka 2030, Tanzania inakiuka lengo la kimataifa la kupunguza vifo vya kina mama, watoto wachanga na watoto wa umri wa chini ya miaka mitano.
Aliyasema hayo jana Jumanne, Februari 4, 2025 alipohutubia wanahabari baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma, kutoka Dar es Salaam, ambako alipokea tuzo hiyo maalum ya kimataifa.
Kulingana naye uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya hasa katika kujenga miundombinu, kununua vifaa tiba, kusomesha wataalamu na kuajiri wahudumu wa afya wa ngazi zote uliwezesha kupungua kwa vifo hivyo vya kina mama na watoto.
Alisema vifo vya kina mama vimepungua kutoka 556 hadi 104 huku engo la kimataifa kwa mwaka 2030 likiwa kufikia vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000.