Rais Ruto: Serikali kutimiza ahadi yake ili kuzuia mgomo wa walimu

Dismas Otuke
2 Min Read
Rais William Ruto.

Rais William Ruto ametoa hakikisho kuwa walimu hawatagoma mwezi huu wakati shule zitakapofunguliwa kwa muhula wa tatu.

Ruto amesema haya leo Ijumaa alipoongoza makala ya 96 ya tamasha la muziki kwa shule  na taasisi za elimu nchini.

Hafla iliandaliwa katika Ikulu ndogo ya Eldoret.

Rais ameweka bayana kuwa serikali imeanza mazungumzo na vyama vya walimu vya KUPPET na KNUT ili kuzuia mgomo wa kitaifa ulioitishwa na vyama hivyo hivi maajuzi.

Walimu wanataka Tume ya Kuwaajiri Walimu, TSC itekeleze kikamilifu nyongeza ya mshahara ya mwaka 2021-2025 kwa mujibu wa Mkataba wa Maelewano (CBA), kupewa bima ya matibabu na kuwasilishwa kwa makato yote ambayo yalitolewa kwenye mishahara ya walimu lakini hayajawasilishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita miongoni mwa matakwa mengine.

Iwapo mgomo wa  walimu utaandaliwa kama ilivyopangwa, basi huenda ukawa tishio kwa mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE iliyoratibiwa kuanza mwezi Oktoba.

Awali, Waziri wa Leba Dkt. Alfred Mutua alitoa wito kwa vyama vya KNUT na KUPPET kuwapatia muda mawaziri wapya kumaizi masuala yanayozikumba wizara zao kabla ya kufanya navyo majadiliano haraka.

Mbali na KNUT na KUPPET, Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege (KAWU) pia kimeitisha mgomo kuanzia Jumatatu wiki ijayo.

“Nina imani kwamba vyama hivyo, vinavyowakilisha maslahi ya wafanyakazi, vinafahamu hali ya sasa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa nchini. Naamini vyama hivyo ni vya kizalendo na vinafikiria mambo yaliyo mbele na kwa hivyo navisihi kukumbatia mazungumzo,” alisema Dkt. Mutua katika taarifa.

 

Website |  + posts
Share This Article