Rais Ruto: Wakenya milioni 12.9 wamejisajili kwa mpango wa SHA

Martin Mwanje
1 Min Read

Jumla ya Wakenya milioni 12.9 wamejisajili na Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA kufikia mwanzoni mwa mwezi huu.

Mamlaka hiyo inasimamia Bima ya Afya ya Jamii, SHIF iiliyochukua mahali pa Bima ya Afya ya Kitaifa, NHIF.

Rais William Ruto ametoa wito kwa Wakenya zaidi kujisajili kwenye mpango huo unaolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote nchini.

Ingawa hospitali zote za umma zimejiunga na mpango huo, ni asilimia 50 pekee ya hospitali za binafsi ambazo zimejiunga.

Rais Ruto ametoa wito kwa hospitali za binafsi ambazo bado hazijajiunga na mpango huo kufanya hivyo ili kuhakikisha Wakenya wote wanapata huduma bora za matibabu.

“Tunatoa wito kwa hospitali za binafsi kuharakisha mchakato wa kutia saini mikataba ili kutuwezesha kumaliza awamu ya mwisho ya utekelezaji wa mpango wa upatikanaji afya kwa wote,” alisema Rais Ruto katika hotuba yake wakati wa sherehe za Siku ya Mashujaa katika kaunti ya Kwale.

“Ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mpango huu, serikali ya Kenya imetoa shilingi bilioni 3 za kulipa madeni ya watoa huduma.”

Rais amewataka Wakenya kukoma kutilia shaka mfumo huo akisema siku chache zijazo, Wakenya watavuna matunda yake kwa Wakenya wote kupata huduma za matibabu.

Share This Article