Rais William Ruto mapema leo Jumatatu alifungua Kongamano la kwanza la Afrika kuhusu Tabia Nchi katika ukumbi wa jumba la mikutano ya kimataifa la Kenyatta, KICC jijini Nairobi.
Ruto aliwarai viongozi wa Afrika kuwekeza zaidi katika mitambo na mashine zinazotumia kawi safi na zisizochafua mazingira na pia kufanya kilimo bora kinachochangia pakubwa utunzaji mazingira.

“Mazungumzo ya Tabia Nchi yalianza mwaka 1992 mjini Rio De Janeiro brazil, ni miaka 31 baadaye ambapo kongamano hilo linaandaliwa Afrika kwa mara ya kwanza,” alisema Ruto.
“Tunao uwezo mkubwa wa kutumia kawi safi na malighafi asilia ambazo zinaweza kutumika vyema bila kuchafua mazingira lakini pia ni lazima tushirikiane kuondoa au kupunguza matumizi ya mashine na mitambo inayotoa gesi ya kabonidioksidi.”

Akihutuba kongamano hilo, Waziri wa Mazingira Soipan Tuya alitilia mkazo kuwa mabadiliko ya tabia nchi na athari zake katika sekta kuu za kiuchumi, kama vile kilimo, ufugaji wa samaki,utalii, nishati,misutu na nyinginezo yanapaswa kutumika kupunguza kukabiliana madeni mengi yanayolikumba bara hili.

Kongamano hilo linafungamana na wiki ya Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi ambayo inaadhimishwa kati ya Septemba 4 na 8 mwaka huu.