Rais William Ruto, ametoa wito kwa wakenya kusitisha majadiliano ya kiholela kuhusu Vikosi vya Ulinzi nchini (KDF), akisema kuwa vikosi hivyo vinapaswa kupewa fursa ya kuhudumu bila mwingilio wowote.
Kutokana na shutuma zilizoelekezwa kwa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi Jenerali Charles Kahariri, kufuatia matamshi yake ya hivi majuzi kwamba KDF haiegemei upande wowote wa kisiasa, kiongozi wa taifa alielezea umuhimu wa kutoingiza siasa katika majukumu ya kijeshi kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.
“Nawahimiza Wakenya wote, viongozi, wanasiasa na wanahabari kwamba wanajeshi wetu ni nguzo kuu ya udhabiti kwa maendeleo ya taifa hili. Tunapaswa kuwa makini na kusitisha matamshi ya kiholela dhidi ya maswala ya kijeshi,” alionya Rais Ruto.
Rais Ruto, ambaye leo Jumatano aliongoza sherehe ya kufuzu kwa maafisa wa kadet katika chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Lanet kaunti ya Nakuru, alihakikisha kuwa utawala wake utaendelea kupiga jeki Vikosi vya Ulinzi katika majukumu yao ya kuhudumia taifa hili.
Kiongozi wa taifa alisema mchango wa KDF kwa maendeleo ya taifa hili hauwezi puuzwa, akidokeza kuwa wanajeshi wanapaswa kupongezwa.
“Utawala wangu na mimi mwenyewe kama amri jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi, nitalinda majeshi yetu kwa vyovyote vile yanapohakikisha udhabiti na maendeleo nchini,” alisema Rais Ruto.
Kulingana na kiongozi huyo wa taifa nguzo muhimu kwa ustawi wa taifa ni pamoja na amani, uongozi bora na maendeleo jumuishi.