Ruto: Sekta ya kibinafsi ni muhimu kufanikisha afya kwa wote

Tom Mathinji
4 Min Read

Rais William Ruto amesema Serikali itashirikiana na sekta ya kibinafsi ili kufanikisha Huduma ya Afya kwa Wote.

Alisema Serikali itaisaidia sekta ya utengenezaji dawa ili kuimarisha uwezo wake wa viwanda vya ndani.

Kiongozi wa nchi alibainisha kuwa Serikali itapitia upya utaratibu wa kodi na gharama za kufanya biashara katika sekta hiyo.

Alisema serikali itaweka kipaumbele kwenye ununuzi wa vifaa vya matibabu kutoka kwa wazalishaji wa ndani ili kusaidia ukuaji wake.

“Uzalishaji wa ndani ni muhimu kwa Huduma ya Afya kwa Wote; kupunguza gharama ya dawa na vifaa vya matibabu kutaifanya kuwa endelevu, nafuu na kuifanya ifanye kazi kwa kila mtu,” alisema.

Rais aliyasema hayo siku ya Jumatano akiwa Syokimau, Kaunti ya Machakos, wakati wa ufunguzi wa Maabara ya MEDS Microbiology.

Kituo hicho cha kisasa kitahudumia na kuendeleza huduma za afya nchini Kenya na kanda.

Waliokuwepo ni Waziri wa Afya Susan Nakhumicha na Naibu Mkurugenzi wa USAID Kenya/ Afrika Mashariki Bert Ubamadu.

Rais Ruto alisema Serikali imetenga ekari 100 kati ya ekari 500 katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Thika kwa makampuni ya kutengeneza dawa.

“Ninawaalika wawekezaji kutumia nafasi hii na kuendeleza viwanda vya utengenezaji bidhaa nchini Kenya,” alisema.

Rais alisema kwamba janga la Korona ni wito wa kuamsha nchi kuimarisha uwezo wake wa utengenezaji bidhaa wa ndani.

Alitoa mfano ambapo nchi zilizuia vifaa vya matibabu kwa matumizi yao ya ndani kwa kuwanyima wale wanaotegemea viwanda hivyo.

“Kuwa na uwezo wa uzalishaji wa ndani ni hakikisho kwetu la ugavi hata wakati ulimwengu unapokabiliwa na nyakati ngumu,” alisema.

Rais alisema Serikali imechukua mtazamo wa jamii nzima katika utoaji wa huduma ili kuhakikisha utoaji wa afya unatoka chini kwenda juu.

“Ajenda yetu ya huduma ya afya lazima iwe shirikishi, ili kufaidika na manufaa ya kipekee ya wadau mbalimbali,” alisema.

Alibainisha kuwa Serikali imeanzisha mageuzi muhimu ya kimuundo na kitaasisi na kutoa uwezo wa kutosha wa rasilimali watu.

Alisema Serikali pia itashirikiana na mashirika ya kidini ili kuhakikisha Wakenya wote wanapata huduma za afya kwa wote.

Rais alisema Serikali inazingatia matumizi ya teknolojia ya hali ya juu ili kukabiliana na ufisadi na utumizi mbaya wa rasilimali za afya.

Hii, alisema, imebadilisha utendakazi katika Mamlaka ya Ugavi wa Dawa ya Kenya.

Alisema teknolojia pia itaimarisha uwazi na uwajibikaji katika Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya ya Jamii (NSHIF), mbeleni iliyojulikana kama Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF).

“Matumizi ya teknolojia yatatusaidia kukabiliana na madai ghushi na wizi na kuhakikisha Kenya inapata thamani kwa kila senti ambayo inachangia,” alisema.

Kwa upande wake Waziri wa afya Susan Nakhumicha, alisema kituo hicho cha MED ni maabara yaliyopitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni.

Alisema itakuza utengenezaji wa ndani wa dawa na pia kuendeleza sifa ya nchi katika sekta hiyo.

“Maabara tunayozindua leo inajaza pengo katika ubora wa bidhaa zinazotengenezwa nchini humu,” alisema.

Bw Ubamadu alisema kituo hicho kitasaidia kulinda Kenya dhidi ya viini vya magonjwa na vitisho vya kiafya katika siku zijazo.

Website |  + posts
Share This Article