Rais Ruto – Kila mtu lazima alipe ushuru

Martin Mwanje
1 Min Read
Rais William Ruto

Kila Mkenya lazima alipe ushuru unaohitajika kwa maendeleo ya taifa hili.

Rais William Ruto ameonya kuwa hakuna atakayependelewa katika wajibu wa ulipaji kodi, haijalishi wadhifa na vyeo wanavyoshikilia katika jamii.

“Ni wajibu wetu sisi sote kama Wakenya kuhakikisha kila mmoja wetu analipa kodi,” alisema Rais Ruto aliyerejelea ujumbe aliopokea kutoka kwa Mkenya mmoja mzalendo akilalamikia hatua ya kampuni moja kukwepa kulipa kodi.

Mkenya huyo alilalama kuwa kampuni huyo ilikwepa kulipa kodi kwa sababu inamilikiwa na watu mashuhuri.

“Haijalishi wewe ni mkubwa kiasi gani, una mamlaka kiasi gani na una nguvu kiasi gani, wamiliki wa kampuni hiyo lazima walipe ushuru kama Wakenya wengine. Hakuna yeyote anayepswa kuitishia Mamlaka ya Ukusanyaji Mapato Nchini, KRA kwa kutumia nyadhifa zao, kujuana kwao na mamlaka yao ili wakwepe kulipa kodi,” alionya Rais Ruto wakati wa maadhimisho ya siku ya ulipaji kodi mwaka 2023 nchini yaliyofanyika jijini Mombasa.

“Lazima sote tulipe kodi, na punde tukilipa kodi, hebu tuitake serikali kutumia kodi yetu kwa njia inayostahili, kuhakikisha haibiwi na haitumiki kifisadi.”

Rais Ruto akitumia fursa hiyo kuonya kuwa wafisadi hawana nafasi katika utawala wake.

 

 

Website |  + posts
Share This Article