Ushirikiano wa kidijitali kati ya China na nchi zinazohusika katika Mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI), ni muhimu kwa maendeleo ya miundombinu.
Rais William Ruto alisema kuna haja ya uwekezaji katika uchumi wa kidijitali kwa ajili ya mabadiliko ya siku za usoni.
“Ninasimama mbele yenu kutoa wito thabiti kwamba jukwaa hili liamue kuwekeza zaidi katika maendeleo ya miundombinu ya Afrika kwa ujumla na hasa kuimarisha uwekezaji katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali barani kote,” alisema Rais Ruto.
Alisema Kenya ndio eneo la kutua kwa nyaya sita za chini ya bahari, kimanufaa kuna kampuni kubwa za kimataifa, utaratibu mzuri wa usafiri barani na kikanda, fursa za kibinadamu, biashara na kivutio cha uwekezaji.
“Kwetu sisi wa jumuiya ya BRI, lazima tukubali kwamba mustakabali wa mabadiliko ni wa kidijitali, na tukubali kujenga juu ya msingi mzuri wa kuunganishwa kwa miundombinu ili kuingia katika dunia hii mpya shujaa,” aliongeza.
Alibainisha kuwa mabadiliko makubwa kwenye majukwaa ya kidijitali yanayofanywa na wazalishaji na watumiaji katika sekta zote na katika kila kiungo cha mtungo wa thamani, pamoja na serikali kukumbatia uwekaji kiotomatiki na kidijitali, bila shaka ni maendeleo ya kichocheo zaidi katika mabadiliko ya kidijitali duniani.
Rais Ruto aliyasema hayo jana Jumatano wakati wa Kongamano la 3 la Ngazi za Juu la Ushirikiano wa Kimataifa la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” mjini Beijing, China.
Aliongeza kuwa mahitaji ya mfumo wa kidijitali, ubadilishanaji mtandaoni, uwasilishaji wa huduma kiotomatiki, na kuongezeka kwa tasnia za kidijitali kulifungua fursa mpya za ajira na kulazimisha mashirika kujipanga upya na kuunda upya.