Rais William Ruto ameangazia tena ongezeko la kutisha la mauaji ya wanawake humu nchini hali anayotaja kuwa ya kusikitisha na isiyokubalika.
Huku akitambua hofu na maumivu wanayopitia wanawake wengi nchini, Rais alisema hali hiyo isiposhughulikiwa itasababisha wanawake nchini kuhisi kwamba hawako salama hata nyumbani.
Alisisitiza haja ya kushughulikia haraka dhuluma za kijinsia ambazo alitaja kuwa namna ya kijadi ya kudhihirisha ukatili ambayo inahujumu maendeleo ya kijamii.
Rais alifichua kwamba ameandaa mazungumzo ya kina na viongozi wa kike kuhusu njia bora za kutokomeza jinamizi hilo huku akitangaza kujitolea kwake kuunga mkono mbinu ya sekta mbali mbali.
Kiongozi wa nchi amewataka wananchi wote kuwajibika katika kuleta mabadiliko ya kitamaduni akisema wakati umewadia wa kila mmoja kukuza wavulana watakaokuwa wanaume bora.
Alitambua umuhimu wa kuimarisha usawa wa kijinsia na kulinda haki ya wanawake kuhusishwa kikamilifu katika utawala.
Rais Ruto alimpa naibu Rais Kithure Kindiki jukumu la kufanikisha juhudi za pamoja kupendekeza mipango itakayotekelezeka ya kutokomeza mauaji ya wanawake katika muda wa miezi sita ijayo.
Kiongozi wa nchi aliyasema haya kwenye hotuba yake kwa bunge kuhusu hali ya taifa, siku moja baada ya mkutano na viongozi wa kike kuhusu suala hilo.
Aliahidi shilingi milioni 100 za kufadhili kampeni dhidi ya uovu huo, itakayotekelezwa wakati wa maadhimisho ya siku 16 za uanaharakati dhidi ya dhuluma za kijinsia.