Rais William Ruto amezindua ujenzi wa nyumba za malazi katika Taasisi ya Kiufundi ya Wumingu, katika kaunti ya Taita Taveta kwenye siku ya kwanza ya ziara yake eneo la Pwani.
Kiongozi wa taifa alisema serikali kuu inawekeza shulingi bilioni mbili katika kaunti ya Taita-Taveta, kujenga nyumba 5,000 za malazi kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu, Taasisi za Kiufundi na wale wa Chuo cha Mafunzo ya Utabibu (KMTC), chini ya mpango wa nyumba za gharama nafuu.
“Nimeweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa nyumba za malazi utakaogharimu shilingi milioni 145 katika Taasisi ya kiufundi ya Wamingu,” alisema Rais Ruto.
Ruto alidokeza kuwa serikali itaweka lami barabara inayotoka Wudanyi mjini hadi kwenye taasisi hiyo,na kuhakikisha upatikanaji wa maji na nguvu za umeme.
Kwenye hafla hiyo, kiongozi wa taifa alisema serikali yake imejizatiti kukamilisha miradi ya maendeleo kama vile elimu, afya na usambazaji wa nguvu za umeme.
Ruto alisema Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA), imelipa shilingi bilioni 1 kwa vituo vya afya katika kaunti ya Taita Taveta na kupunguza gharana ya natibabu kwa wakazi wa eneo hilo.
Rais Ruto ameanza ziara ya maendeleo katika eneo la Pwani leo Jumamosi, ambapo anatarajiwa kuzuru kaunti za Taita Taveta, Kwale, Kilifi, Mombasa, Tana River na Lamu.
Wakati wa ziara hiyo, Rais anatarajiwa kukabidhi hatimiliki laki mbili za ardhi huku 31,318 zikikabidhiwa wakazi wa maeneo bunge ya Mwatate na Voi kwenye gatuzi la Taita Taveta.