Wakenya waonywa dhidi ya siasa za migawanyiko

Tom Mathinji
1 Min Read
Musalia Mudavadi - Mkuu wa Mawaziri.

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ametoa wito kwa Wakenya kudumisha amani, kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kukataa siasa za migawanyiko.

Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa la Redeemed lililoko katika barabara ya Likoni jijini Nairobi, Mudavadi alihimizi mazungumzo badala ya migawanyiko, huku akipigia debe umoja kupitia matamshi yanayotolewa.

“Kama Wakenya, ni sharti tuchague kushiriki mazungumzo badala ya migawanyiko, maelewano badala ya hasira. Matamshi yetu yaweze kutuunganisha jinsi tu yanavyoweza kututenganisha,” alisema Mudavadi.

Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alihimiza umuhimu wa kuwa na jamii yenye amani, taifa lililojikita kwa maadili yanayovutia uwekezaji na kutoa fursa kwa ukuaji.

Wakati huo huo, Mudavadi aliwataka wananchi kujiandikisha kuwa wapiga kura na kujiandaa kushiriki kwa amani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Alisisitiza kwamba kura inasalia kuwa chombo chenye nguvu zaidi cha kidemokrasia cha kuamua uongozi, akiwahimiza Wakenya kukataa vurugu na hali ya kutovumiliana kisiasa.

Share This Article