Serikali ya Uganda, imetangaza mipango ya kuwarejesha nyumbani raia wake kutoka Afrika kusini, kufuatia ghasia zinazowalenga raia wa kigeni zinazoendelea kushuhudiwa Afrika Kusini.
Kupitia kwa taarifa Jumapili jioni, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Haruna Kasolo, alisema Rais Yoweri Museveni ameagiza serikali kuwarejesha nyumbani raia wa Uganda wanaokabiliwa na hatari ya kiusalama Afrika Kusini.
Kulingana na Kasolo, raia 746 tayari wamejiandikisha kurudi nyumbani na kwamba wizara hiyo ilikuwa ikishirikiana na mashirika husika ya serikali, jamii ya Uganda nchini Afrika Kusini, na Ubalozi Mkuu wa Uganda huko Pretoria ili kukamilisha mpango wa kuwahamisha.
Kasolo alisema serikali itawezesha usajili wa wanaorejea, kuwahamishia kwenye vituo salama vya kukutana, kutoa hati za usafiri wa dharura inapobidi, na kuondoka kwao kutoka Afrika Kusini.
Aidha amesema shirika la ndege la Taifa la Uganda, litaendesha ndege maalum za kukodi kwa ajili ya kuwarejesha nyumbani, huku gharama zikibebwa na serikali ya Uganda.
Kasolo aliwasihi Waganda wanaotaka kurudi nyumbani kujiandikisha kwenye Ubalozi Mkuu wa Uganda huko Pretoria haraka iwezekanavyo.
Wakati huo huo, serikali ya Uganda imesema kuwa raia wengine wa Uganda waliondoka Afrika Kusini kabla ya kukamilika kwa makataa ya Juni 30, 2026, yaliyotolewa kwa raia wa kigeni kuondoka Afrika Kusini.