Rais William Ruto amewataka watu wote ulimwenguni kuwa na ujasiri na kubuni mipango ya kimkakati katika harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kiongozi huyo wa nchi alisema kwamba wakati umewadia wa kuchukua hatua mwafaka katika kubadili mifumo hitajika ya kuweka kiwango kinachokubalika cha ongezeko la joto duniani kuwa nyuzi joto 1.5.
Alitaka watu wa mabara ya Afrika, Ulaya na eneo zima kushirikiana katika kupunguza kwa kiwango kikubwa gesi chafu.
“Hilo litasababisha ufanisi kwa kila mmoja.” alisema Rais.
Aliyasema hayo Jumanne huko Strasbourg, Ufaransa, alipohutubia bunge la Umoja wa Ulaya.
Rais alitaka mabadiliko yafanywe kwenye mifumo ya miungano na ushirikiano wa kimataifa akisema mifumo ya miungano hiyo na taasisi za kimataifa iliyobuniwa katika karne ya 20 imepitwa na wakati.