Jaji Mkuu Koome ataka kesi za dhuluma za kingono kuharakishwa

Marion Bosire
2 Min Read

Jaji Mkuu Martha Koome anataka kasi ya kusikiliza na kuamua kesi za dhuluma za kingono na kijinsia izidishwe. 

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa awamu ya kwanza kabisa ya kongamano la kitaifa kuhusu dhuluma za kingono na kijinsia jijini Nairobi, Koome alisema kwamba visa hivyo vya dhulma vimeongezeka sana na kuendesha kesi kama hizo pole pole kunaathiri sana wanaonusurika.

Mandhari ya kongamano hilo ni “Kuimarisha utekelezaji na upatikanaji wa haki kwa waathiriwa wa dhuluma za kingono na kijinsia”.

Jaji mkuu alisema dhuluma hizo husababishia wahusika athari za kimwili, kiakili na kihisia na baadaye kusababisha unyanyapaa, kudharauliwa na kutengwa na jamii.

Alisema suluhisho kwa hali hiyo ni walezi wa sheria na ufanisi wa mwingilio wa asasi za sekta ya haki ili kuziba pengo lililopo kati ya matatizo ya waathiriwa na matumaini ya maisha bora siku za baadaye.

“Lazima tuangazie namna ya kuimarisha uwezo wetu wa kusimamia na kulinda ushahidi ambao ndio sauti kuu inayoelezea matukio hayo. Hii inahitaji uhusiano mwema na mashahidi na usimamizi bora wa ushahidi kulingana na viwango hitajika vya sera bora za kikazi.” alisema Koome.

Msimamizi huyo wa idara ya mahakama alihakikishia wakenya kujitolea kwa sekta hiyo kuimarisha ufanisi wao katika kushughulikia kesi za dhuluma za kingono na kijinsia.

Ili kufanikisha hilo, alisema idara ya mahakama mwezi Juni, ilizindua mfumo wa mabadiliko ya kijamii kupitia kwa mkakati wa upatikanaji wa haki katika dhuluma hizo mahakamani.

Mahakama 12 za dhuluma za kingono na kijinsia zimezinduliwa kote nchini hasa katika maeneo yanayokabiliwa na visa vya dhuluma za kingono na kijinsia kufuatia kufanikiwa kwa mradi anzilishi huko Shanzu, Mombasa.

Kulingana na takwimu kuhusu idadi ya watu na afya za mwaka 2014 za afisi ya kitaifa ya takwimu KNBS, asilimia 45 ya wanawake na wasichana wa umri wa kati ya miaka 15 na 49 wamedhulumiwa kimwili huku asilimia 14 kati yao wakidhulumiwa kingono.

Website |  + posts
Share This Article