Rais Ruto: Wanawake ni nguzo kuu ya uongozi wa nchi

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto amewalimbikizia sifa wanawake akiwataja kuwa nguzo kuu katika uongozi na siasa za nchi. 

Amewataja wanawake kuwa watu jasiri akitoa mfano wa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na mwenzake wa Embu Cecily Mbarire waliofanya uamuzi mgumu wa kumuunga mkono wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.

“Miongoni mwa watu waliofanya maamuzi yaliyonithibitishia kuwa wanawake ni jasiri ni uamuzi uliofanywa na Waiguru kujiunga na timu yetu. Alipojiunga na timu yetu, sikuamini. Ni uamuzi uliotokana na ujasiri mwingi,” alisema Rais Ruto katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa mkakati wa vuguvugu la Wanawake 7 Magavana, G7 nchini.

Uzinduzi huo ulifanyika katika hoteli moja jijini Nairobi leo Alhamisi.

G7 ni vuguvugu linalowaleta pamoja Magavana Anne Waiguru wa Kirinyaga, Susan Kihika wa Nakuru, Wavinya Ndeti wa Machakos, Fatuma Achani wa Kwale, Kawira Mwangaza wa Meru na Cecily Mbarire wa Embu

“Wanawake ndio nguzo ya siasa za nchi yetu. Wao ndio wanaongoza mabadiliko na daraja kuelekea maongozi ya kidemokrasia,” aliongeza Rais Ruto.

Aliahidi kufanya kila awezalo kuhakikisha ushiriki wao katika uongozi wa nchi.

Website |  + posts
Share This Article