Mshukiwa wa ugaidi auawa nchini Uganda

Alikabiliwa na kumalizwa katika soko la Kalerwe lenye shughuli nyingi karibu na barabara ya Kaskazini pembeni mwa jiji la Kampala.

Marion Bosire
1 Min Read

Taarifa ya jeshi la watu wa Uganda inasema kwamba mshukiwa wa ugaidi wa kike, mshambuliaji wa bomu wa kujitoa mhanga kufa, aliuawa jijini Kampala Jumapili asubuhi.

Kulingana na jeshi, mwanamke huyo alikabiliwa na kumalizwa katika soko la Kalerwe lenye shughuli nyingi karibu na barabara ya Kaskazini pembeni mwa jiji la Kampala.

Jeshi lilichapisha picha mitandaoni ya mwili wa mwanamke huyo ukiwa umefunikwa na begi jeusi likiwa kando yake, na kuelezea kwamba wanajeshi wenye ujuzi kuhusu mabomu walifika katika eneo la tukio.

Haya yanajiri wiki tatu tu baada ya mshambuliaji mwingine wa kujitoa mhanga kufa, kuuawa alipokuwa akijaribu kushambulia kanisa la Munyonyo Minor Basilica, ambapo waumini wengi walikuwa wakisherehekea siku ya wafia dini.

Kaimu msemaji wa jeshi la Uganda Kanali Chris Magezi, alimtambua mshukiwa wa siku hiyo kama Aisha Katushabe, ambaye pia hujulikana kwa majina mengine kama Byaruhanga Sumayya na Kabonesa .

Katushabe ambaye anaaminika alikuwa na umri wa miaka ishirini hivi, aliviziwa na maafisa mita 600 kutoka kanisa la Munyonyo na bomu alilokuwa amebeba likaharibiwa.

Aliwahi kukamatwa mwaka 2023 kwa makosa yanayohusiana na ugaidi kisha kaachiliwa kwa ukosefu wa ushahidi, anaaminika kwa na uhusiano na kundi la Allied Democratic Forces – ADF nchini DRC.

Website |  + posts
Share This Article