Rais Ruto awaonya wafisadi, awataka kubadili dira la sivyo waadhibiwe

Martin Mwanje
3 Min Read
Rais William Ruto akiwahutubia viongozi wa magharibi katika Ikulu Ndogo ya Kakamega

Rais William Ruto amesema azimio la kupigana na ufisadi nchini litaendelea hadi jinamizi hilo liangamizwe.  

Amesisitiza kuwa wafisadi lazima wakomeshe uovu huo au waadhibiwe.

Rais amesema Kenya imeathiriwa vibaya na ufisadi, wizi na utumizi mbaya wa rasilimali za umma.

“Hatuwezi tukakubali ufisadi kuendelea. Tunahitaji kutafuta suluhu ya kudumu. Wezi wote ni sharti wasitishe vitendo vyao.”

Aliwaonya wale wanaotumia siasa na mahakama kuwalinda wezi akiongeza kuwa wakati wao umekwisha.

“Hakuna mahali pa watu kama hao kujificha. Badilika, ondoka Kenya au uende jela.”

Rais Ruto aliyasema hayo leo Jumatano katika Ikulu Ndogo ya Kakamega alipofanya mkutano wa mashauriano na viongozi wa magharibi mwa nchi wakiongozwa na Waziri Mwenye mamlaka Makuu Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha na Magavana Fernandes Barasa (Kakamega), Paul Otuoma (Busia), Wilber Ottichilo (Vihiga) na Ken Lusaka (Bungoma) ni miongoni mwa viongozi waliokuwapo.

Rais alisema hivyo siyo vitisho bali wito wa kuchukuliwa kwa hatua.

Aliuambia mkutano huo kuwa alipigwa na butwaa kwamba yeyote humu nchini anaweza akatetea ufisadi.

“Hatuwezi tukatetea kile ambacho kimeifanya Kenya kurudi nyuma.”

Aidha aliuambia upinzani kuwacha kupoteza wakati ukitetea wezi na kuahidi kupigania sekta ya sukari iliyojaa matapeli.

“Tutailainisha sekta yote ya sukari kwa sababu tunatumia pesa nyingi kuagiza sukari,” alieleza Rais.

Aliongeza kuwa serikali itafufua sekta ya sukari nchini “ili tuweze kuzalisha sukari humu nchini na kusaidia kukuza uchumi wetu”.

Alipendekeza kuanzishwa kwa viwanda zaidi vya kusaga miwa ili kuvisaidia vilivyopo katika uzalishaji.

Kadhalika alitoa wito kwa viongozi kufanya kazi pamoja katika kuibadilisha Kenya.

Kwa upande wake, Gachagua alisema Kenya ipo kwenye njia ya kufufua na kukuza uchumi wake.

“Tutafanya kazi na viongozi wote kubadilisha maisha ya Wakenya,” alisema Gachagua.

Mudavadi alilitaka eneo la magharibi kuiunga mkono serikali.

“Hapa ndipo ulipo mustakabali wetu.”

Baadaye, Rais Ruto alizindua kiwanda cha kuongezea thamani cha kaunti ya Kakamega katika eneo la Likuyani.

Pia alifungua rasmi Chuo cha Mafunzo ya Tiba cha Kenya, KMTC bewa la  Navakholo ambacho aliweka jiwe lake la msingi mnamo mwezi Julai mwaka 2018.

Share This Article