Waziri wa vyama vya ushirika Wyclife Oparanya amerai vyama vya maziwa nchini kukumbatia ushirikiano ili kulinda wakulima dhidi ya ushindani usiofaa. Akihutubia baadhi ya viongozi wa vyama hivyo na wakulima kwenye kiwanda kipya cha maziwa ya KCC katika Kaunti ya Meru, Oparanya alisema haja kuu ya wakulima ni soko na bei bora ya huku akitaka kiwanda hicho kushirikiana na viwanda vingine vipya vilivyoko eneo hilo kwa lengo la kuongeza usambazaji na uzalishaji wa maziwa.
“ Viwanda vyote vinavyomilikiwa na wakulima na watu binafsi vinanawiri kuliko vile vya serikali, usambazaji na usindikaji katika kiwanda cha serikali ni wa mwendo wa kobe ”, Alisema Oparanya.
Pia aliwataka wakulima kuamini katika mabadiliko yanayoendelea kwenye sekta hiyo kwani tayari yamezaa matunda ambapo wakulima wanalipwa siku ya kwanza ya mwezi.
“Nimeupa usimamizi wa New KCC siku 90 kubadilisha kiwanda hiki ili kitoe faida itakayo badilisha raslimali ya watu, kuongeza uzalishaji wa bei kwa lita hadi shilingi 55, kupunguza siku za malipo hadi wiki mbili na kupea kipaumbele maslahi ya wakulima’’, Alieleza Oparanya.
Hata hivyo, alilalama kuhusu kutotumika kwa kituo kipya cha New KCC cha mjini Nyambene ambacho kiligharimu shilingi milioni 500.
Vile vile, waziri alishiriki kikao na bodi ya usimamizi ya chama cha ushirika cha Meru ya kati kinachozalisha maziwa ya Mount Kenya. Akiwa huko, alisifia sekta ya maziwa ambayo imeboresha maisha ya zaidi ya watu milioni moja.
Naye mkurugenzi mkuu wa kampuni ya maziwa ya Mount Kenya Kenneth Gitonga, alikumbatia hatua ya serikali ya kuinua wakulima wa nyanjani kupata soko na bei nzuri ya maziwa.