Rais William Ruto ameongoza taifa kuwaomboleza waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea eneo la Londiani kaunti ya Kericho Ijumaa jioni.
“Ni swala la kutamausha kwamba baadhi ya waliofariki ni vijana na wanabiashara waliokuwa katika shughuli zao za kila siku. Waliojeruhiwa tunawaombea afueni ya haraka. Tunawahimiza madereva kuwa waangalifu zaidi, hasaa wakati huu wa msimu wa mvua,” alisema Rais Ruto.
Viongozi wengine walioomboleza na familia za waathiriwa ni pamoja na naibu Rais Rigathi Gachagua, aliyesikitika kuwa ajali hiyo imesababisha hasara kubwa kwa taifa hili.
“Ni uchungu mwingi sana kuwapoteza wapendwa katika umi wowote ule, hasaa kupitia ajali ya barabarani kama hii. Tunazifariji familia zilizopoteza wapendwa wao, huku tukiwatakia afueni waliojeruhiwa. Nawahimiza wanaotumia barabara kuwa waangalifu zaidi,” alisema Naibu Rais.
Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen alituma risala za rambirambi kwa familia za waathiriwa wa ajali hiyo. Aidha alisema uchunguzi utafanywa kubaini klichosababisha ajali hiyo.