Rais William Ruto leo Jumanne, amekabidhi hati za kuhudumu kwa chuo kikuu cha Islamic humu nchini na chuo kikuu cha kitaifa cha ujasusi na utafiti kwenye hafla iliyoandaliwa katika Ikulu ya Nairobi.
Akizungumza wakati wa sherehe hiyo rais aliiagiza tume ya elimu ya juu kuhakikisha viwango vya elimu viazingatiwa kuambatana na mahitaji ya sekta hiyo.
Alikitaka chuo hicho kikuu cha ujasusi na utafiti kutumia utafiti na teknolojia ili kuwawezesha maafisa wa kijasusi kukabiliana na uhalifu wa kimtandao, ugaidi na changamoto nyingine za kiusalama duniani.
Wakati huo huo alitetea mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu akisema unahakikisha usawa katik elimu ya juu na pia kushughulikia changamoto za ufadhili katika vyuo vikuu.
Kwa upande wake, naibu rais Kithure Kindiki alikitaka chuo kikuu cha Islamic kulinda dhidi ya uenezaji wa itikadi kali na utumiaji dini kwa njia isiyofaa kupitia dhana potovu.
Mkurugenzi mkuu wa huduma ya kitaifa ya ujasusi, Noordin Haji, alisema kuwa kukabidhiwa kwa hati hiyo kutahakikisha kwamba maafisa wa kijasusi wana ujuzi zaidi wa kushughulikia vitisho changamani vya kiusalama.