Rais William Ruto amewasili mjini Arusha nchini Tanzania kuhudhuria Mkutano usiokuwa wa Kawaida wa 25 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo utaangazia mpango wa ufadhili endelevu wa nchi nane wanachama wa jumuiya hiyo.
Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki pia itajadiliwa wakati wa mkutano huo wa siku mbili.
Ruto atajumuika na Marais wenzake Samia Suluhu wa Tanzania ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo, Salva Kiir (Sudan Kusini ambaye ni mwenyekiti anayeondoka wa jumuiya hiyo), Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Evariste Ndayishimiye (Burundi), Felix Tshisekedi (DRC) na Hassan Sheikh (Somalia).
Mkutano huo unafanyika wakati maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa tena kwa EAC pia yanaandaliwa.
“Tunapaswa kutumia ipasavyo fursa zinazoibuka na kujenga EAC ambayo ni thabiti zaidi na yenye ushindani abayo itaharakisha kuanzishwa kwa soko moja la Afrika,” amesema Ruto.
Kwenye taarifa awali, msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed alisema wakati wa mkutano huo, Rais Ruto atajadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya pamoja ya kiuchumi, kuimarisha juhudi za kanda za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuangazia ukosefu wa usalama.
“Rais Ruto atapigania kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara, kuimarishwa kwa biashara za kuvuka mpaka na kuongezwa kwa ushirikiano katika nyanja za nishati, kilimo na ubunifu wa kidijitali ili kubuni nafasi za ajira na kuongeza vyanzo vya mapato,” alisema Mohamed.
“Viongozi pia watazungumzia hatua za kupigia chapuo amani na usalama, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na uhalifu wa kimataifa, kusimamia mipaka na kutatua migogoro.”
Leo Ijumaa alasiri, Rais Ruto atashiriki kikao cha kuadhimisha miaka 25 tangu kuasisiwa kwa EAC.
Aidha, Rais atafanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi wa kanda hii pembezoni mwa mkutano huo.