Rais William Ruto ametetea hatua yake ya kutia saini kuwa sheria Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Kimtandao wa mwaka 2024.
Akizungumza leo Alhamisi wakati wa mazishi ya baba yake Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja, Mzee Weston Kirocho Kanja, katika kaunti ya Laikipia, Rais Ruto ametoa wito kwa wale wanaokosoa sheria hiyo kusema ukweli.
Ruto pia akionekana kuwajibu wale wanaomkosoa kwa kutia saini kuwa sheria miswada minane Oktoba 15 wakati ambapo taarifa za Waziri Mkuu Raila Odinga kufariki wakati akipokea matibabu nchini India zilikuwa zimezagaa.
“Marekebisho yalianza mwaka 2024 na yalifanywa na bunge. Mimi niliamka Jumatano kwa sababu hiyo ndio ilikuwa kazi yangu ya siku hiyo, na ni kazi ya kikatiba ya kutia saini sheria kwa sababu ilikuwa imepita viwango vyote, nikaletewa na Spika. Bahati mbaya tukapoteza Waziri wetu Mkuu wa zamani. Lakini tayari nilikuwa ofisi kwa hiyo kazi,” alibainisha Ruto.
“Hakuna kitu cha kuficha, hakuna kitu cha giza, hakuna kitu kinafanywa usiku, tunafanya kitu sahihi kwa ajili ya Kenya. Tunataka kulinda nchi hii kutoka hali zinazodhoofisha hali ya vijana wa nchi yetu, hali ya Wakenya, usalama wa nchi na yale mambo mengine ambayo yatatusaidia. Wale wanaosema waseme ukweli.”
Ingawa Rais Ruto alitia saini miswada minane kuwa sheria, Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Kimtandao wa mwaka 2024 umemulikwa mno huku wakosoaji wakidai unalenga kukandamiza haki ya Wakenya kujieleza, mbali na mashaka mengine.
Miswada mingine iliyotiwa saini na Rais Ruto ni pamoja na ule wa Marekebisho ya Sheria ya Tume ya Ardhi wa mwaka 2023, Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ardhi wa mwaka 2024, na Mswada wa Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyama Pori wa mwaka 2023.
Mingine ni ule wa Marekebisho ya Sheria ya Tume ya Huduma za Polisi wa mwaka 2024, Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ada za Usafiri wa Anga wa mwaka 2025, Mswada wa Watoaji Huduma za Mali Mtandaoni wa mwaka 2025 na Mswada wa Ubinafsishaji wa mwaka 2025.
Wakati akiitia saini miswada hiyo, Rais Ruto alisema sheria hizo mpya zinatarajiwa kushughulikia dhuluma za kihistoria, kuleta usawa na uwazi na kupiga jeki ajenda ya ustawi na mageuzi humu nchini.
