Rais Ruto atakiwa kumteua Joho mgombea mwenza 2027

Viongozi wa Pwani wanasema Rais Ruto atapata asilimia 99 ya kura mwaka 2027 kutoka eneo la Pwani ikiwa tu atamteua Joho kama mgombea mwenza.

radiotaifa
2 Min Read

Taarifa ya Martin Mwanje na Dickson Wekesa

Viongozi wa Pwani wamezidisha wito wao wa kutaka Waziri wa Madini Hassan Joho kuteuliwa kama mgombea mwenza wa Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Wakiongozwa na Gavana wa Mombasa ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM Abdulswamad Nassir, viongozi hao wamesema shabaha yao kuu ni kupata wadhifa wa Naibu Rais.

“Nazungumza kwa niaba ya chama cha ODM kwamba tutawasilisha wagombea katika nyadhifa zote kuanzia kwa MCA hadi Gavana na ikiwa mazungumzo yetu na UDA yataendelea vizuri, basi wadhifa wa Naibu Rais utakuwa wetu na mtu atakayechukua wadhifa huo ni Hassan Joho,” alisema Gavana Nassir.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kundi la Wabunge wa Pwani ambaye pia ni Mwakilishi wa Wanawake wa Kilifi Getrude Mbeyu alisema Ruto atapata asilimia 99 ya kura mwaka 2027 kutoka eneo la Pwani ikiwa atamteua Joho kama mgombea mwenza wake.

“Tutampa Ruto asilimia 99 ya kura zetu ikiwa tu atamteua Joho kama mgombea mwenza wake na mwaka 2032, tutahakikisha kwamba Joho anagombea urais,” aliongeza Mbeyu.

Wawili hao waliyasema hayo katika shule ya upili ya Town mjini Malindi wakati wa usambazaji wa chakula kilichotolewa na Shirika la Hassan Joho.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri Joho, Naibu Gavana wa Kilifi Flora Chibule, wabunge Badi Twalib wa Jomvu, Rashid Benzima wa Kisauni, Amina Mnyazi wa Malindi, Mishi Mboko wa Likoni na Seneta wa Mombasa Mohamed Faki.

Kauli zao zinawadia wakati ambapo viongozi wa Mlima Kenya wamesimama kidete na kusema kamwe wadhifa wa Naibu Rais si wa kubishaniwa kwani utaendelea kushikiliwa na eneo hilo.

Wadhifa huo ulishikiliwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kabla ya kubanduliwa.

Kwa sasa unashikiliwa na Prof. Kithure Kindiki ambaye pia ameonekana kupuuzilia mbali jitihada za ODM za kumezea mate wadhifa huo.

Share This Article