Rais Ruto asisitiza kujitolea kuhakikisha huduma bora za afya

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amesisitiza kwamba serikali imejitolea kuhakikisha kwamba kila Mkenya anafurahia huduma bora za afya.

Kulingana na kiongozi huyo wa nchi, juhudi kwa sasa zinaangazia mabadiliko chini ya Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA.

Akizungumza katika kanisa la St. Marys’ AIPCA Kathelwa, kaunti ya Meru wakati wa ibada ya Jumapili, Rais alielezea kwamba chini ya huduma msingi za afya, Mkenya anaweza kuingia kwenye kituo chochote cha afya cha umma.

Anapofika huko, ana haki ya kupokea matibabu, kupatiwa dawa na kuruhusiwa kwenda nyumbani bila kulipa pesa zozote.

Ruto amewataka Wakenya kutokubali kulaghaiwa na wahudumu wanaotaka kujipatia faida haramu kwa kuwalazimisha kulipia huduma ambazo tayari zinatolewa na serikali bila malipo.

Vile vile, ameahidi kwamba serikali itakamilisha miradi yote iliyokwama kote nchini ili kuhakikisha utoaji huduma kwa wananchi unaimarishwa.

Website |  + posts
Share This Article