Rais William Ruto amesifia maandalizi yaliyofanikiwa ya awamu ya 72 ya mashindano ya uendeshaji magari ya WRC Safari Rally, katika mbuga ya Hell’s Gate huko Naivasha.
Katika hotuba yake ya kufunga mashindano hayo rasmi, kiongozi wa nchi alitaja mashindano hayo kuwa dhihirisho la mapenzi ya wakenya kwa mashindano hayo na ukuaji wa sifa za taifa hili kama eneo bora la michezo ulimwenguni.
Rais Ruto alipongeza washiriki wote, akitambua njia yenye changamoto waliyokuwa wakitumia pamoja na hali isiyotabirika ya hewa, masuala yaliyoweka kwenye mizani ujuzi wao.
Alisisitiza kwamba kila mmoja aliyeshiriki mashindano ni bingwa wa ukweli kwa kukiuka njia yenye changamoto nyingi.
“Kenya inajivunia maandalizi ya mashindano haya, ambayo yameonyesha mapenzi ya wakenya kwa mashindano ya magari na yamekuwa na athari kubwa kwa uchumi wetu, kutoa fursa za kazi na ubadilishanaji wa fedha za kigeni.
Mashindano hayo yaliyovutia watu wa mataifa 20 na washindani 48 yaliangazia pia uwezo wa Kenya wa kuandaa mashindano ya kiwango cha kimataifa kama mashindano ya soka barani Afrika.
Rais Ruto alitaja pia kujitolea kwa Kenya kuhakikisha usalama akitambua kufanikiwa kwa mpango wa kofia za kujikinga almaarufu helmet na ushirikiano wa Kenya na wakfu wa FIA na AA Kenya kuhimiza usafiri salama.
Ruto alimalizia kwa kualika kila mmoja kwa awamu ya 73 ya mashindano hayo ya WRC Safari Rally mwaka 2026, huku akishukuru waandalizi, wadhamini, idara za serikali na mashabiki.