Rais William Ruto anashiriki kiamsha kinywa na wanariadha wa Kenya walionyakua nishani katika michezo ya Olimpiki iliyokamilika hivi maajuzi jijini Paris nchini Ufaransa.
Kikao hicho kinahudhuriwa na wanariadha walioishindia Kenya medali miaka ya awali akiwemo Ezekiel Kemboi, maafisa wa shirika la riadha la Kenya na maafisa wa wizara ya michezo.
Waziri mpya wa masuala ya michezo Kipchumba Murkomen na katibu katika wizara hiyo pia wanahudhuria kikao hicho katika ikulu ndogo ya Eldoret.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Rais wa kamati ya Olimpiki nchini Paul Tergat alisifia wanariadha walioshiriki michezo ya Olimpiki mwaka huu akisema walijikakamua.
Hata ingawa idadi ya medali ilipungua pakubwa Tergat alisema timu ya Kenya iliibuka nambari moja katika bara Afrika kwa wingi wa medali.
Alisema wanaanza kujiandaa kwa mashindano yajayo ya kimataifa mara moja ili kuirejeshea Kenya hadhi yake katika riadha ulimwenguni na wanatumai kufanya vyema katika michezo ya Olimpiki ya vijana mwaka 2026 jijini Dakar nchini Senegal.
Tergat aliombea mashirika ya michezo nafasi za afisi hasa katika viwanja vya michezo kama Nyayo na Kasarani ili maafisa waweze kushughulikia wanariadha kwa urahisi.
Rais wa shirikisho la riadha la Kenya Jackson Tuwei kwa upande wake alitambulisha washindi wa medali katika michezo ya Olimpiki mwaka huu, akisema haya ndiyo matokeo ya tatu kwa ubora katika Olimpiki tangu Kenya ilipoanza kushiriki mwaka 1956.