Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ametoa wito kwa ushirikiano wa kikanda ili kukabiliana na ueneaji wa silaha haramu.
Akizungumza leo Ijumaa wakati wa zoezi la kuharibu zaidi ya silaha haramu 6,000 katika kaunti ya Kajiado, waziri huyo alisema juhudi za kutwaa silaha haramu zinapaswa kupigwa jeki na juhudi kutoka mataifa jirani.
“Iwapo tunataka kukabiliana na silaha ndogo ndogo na tatizo la ukosefu wa usalama katika kanda hii, imebainika kuwa haitakuwa sawa kutwaa silaha katika nchi moja na kuacha nchi jirani,” alisema Murkomen.
“Ushirikiano wa kikanda katika kutwaa silaha haramu kutoka kwa wananchi ndoio njia ya pekee ya kuhakikisha nchi yetu ni salama,” alidokeza waziri huyo.
Alipongeza operesheni ya Maliza Uhalifu, kwa ufanisi wake katika kupunguza visa vya ujangili kwa hadi asilimia 70, tangu Rais William Ruto alipochukua hatamu za uongozi wa taifa hili.