Rais Ruto apongeza Wakenya walioshiriki Chicago Marathon

Amos Kipruto alishinda mbio za wanaume kwa muda bora zaidi katika rekodi yake binafsi wa saa 2:01:09

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amepongeza wanariadha wa Kenya kwa kufanya vizuri katika mbio za Chicago Marathon za mwaka 2026, ambapo nchi hiyo ilitwaa ubingwa wa wanaume na kushinda nafasi nyingine kadhaa za jukwaani.

Katika taarifa yake ya kuwapongeza wanariadha hao, Rais Ruto alieleza fahari ya taifa kutokana na mafanikio hayo.

“Tunaipongeza Timu ya Kenya kwa kutufanya tujivunie katika mbio za Chicago Marathon. Hongera Amos Kipruto kwa kushinda mbio za wanaume kwa muda bora zaidi katika rekodi yake binafsi wa saa 2:01:09,” alisema Ruto.

Ushindi huo wa Kipruto umeweka rekodi ya muda wa pili wa kasi zaidi kuwahi kutumika na mshindi katika historia ya mbio za Chicago Marathon.

Rais huyo pia aliwapongeza wanariadha wa Kenya waliofanya vizuri katika mbio za wanawake, ambapo nchi hii ilipata nafasi mbili za jukwaani baada ya ushindani mkali katika kilomita za mwisho.

“Pia tunawapongeza Sharon Lokedi na Brigid Kosgei kwa kumaliza katika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia katika mbio za wanawake,” aliongeza Rais Ruto.

Lokedi alivuka mstari wa mwisho kwa muda wa saa 2:14:07, akifuatiwa kwa karibu na Kosgei, ambaye aliwahi kushikilia rekodi ya dunia.

Mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha sifa ya Kenya kimataifa kama taifa lenye nguvu katika mbio za masafa marefu.

Share This Article