Rais William Ruto, ametoa wito wa kuunganishwa kwa michakato ya amani ya Nairobi na Luanda ili kushughulikia kwa pamoja ghasia zinazoghubika Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.
Akizungumza wakati wa mkutano wa ngazi za juu kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Shirika la Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ulioongozwa kwa pamoja na Rais Ruto na mwenzake wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi wa taifa alielezea umuhimu wa kuuganisha michakato hiyo ya amani katika kuafikia udhabiti endelevu katika kanda hii.
“Leo tutaangazia pendekezo la kuunganisha michakato hiyo miwili, majukumu ya wapatanishi na juhudi jumuishi za upatanishi kuhusu mashariki mwa DRC,” alisema Rais Ruto.
Wataalam wa kiufundi kutoka EAC, SADC, na AU wamebuni mapendekezo kuhusu kuunganishwa kwa michakato hiyo, kuambatana na maagizo ya hapo awali ambayo yatatoa mwongozo kwa kundi la wapatanishi.
Rais Ruto alipongeza mafanikio ya kidiplomasia ya hivi majuzi kupitia juhudi za Lunda na Washington, zilizosababisha kujitolea kutoka kwa pande husika kukabiliana na mzozo huo, huku akiwashukuru viongozi kwa juhudi zao.
Waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Marais wastaafu Olusegun Obasanjo (Nigeria), Uhuru Kenyatta (Kenya), Catherine Samba-Panza (Afrika ya Kati) Sahle-Work Zewde (Ethiopia) na Dkt. Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi (Botswana).