Rais Ruto amteua Raila Odinga kuwa Mjumbe Maalum wa Sudan Kusini

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais Ruto amteua Raila Odinga kuwa mjumbe maalum wa Sudan Kusini.

Rais William Ruto amemteua Raila Odinga kuwa mjumbe maalum wa Kenya nchini Sudan Kusini, katika juhudi za kutatua mgogoro unaoghubika taifa hilo, hasaa baada ya kuzuiliwa kwa Makamu wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Riek Machar.

Uteuzi huo umetangazwa leo Ijumaa na katibu katika wizara ya Mambo ya Nje Korir Sing’Oei, aliyesema kuwa Raila anatarajiwa kusafiri Sudan Kusini leo Ijumaa kwa mazungumzo ya amani na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na Makamu wa Rais Riek Machar.

“Rais William Ruto, ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amemteua Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kuwa mjumbe wake maalum Sudan Kusini,” alisema Sing’Oei kupitia ukurasa wa X.

Rais Ruto amemteua Raila siku moja baada ya kuzungumza kwa njia ya simu na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, kujadili mchakato wa kusuluhisha mzozo unaokumba taifa hilo.

“Nilizungumza kwa njia ya simu na Rais Salva kiir, kuhusu kukamatwa na kuzuiliwa kwa Makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar,” alisema Rais Ruto kwenye ukurasa wa X.

Dkt Machar alikamatwa siku ya  Jumatano na maafisa wa usalama waliovamia makazi yake mjini Juba na kuwapokonya silaha walinzi wake na kisha kumzuilia.

Kufuatia kukamatwa kwake, Machar aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi pamoja na mkewe, Angela Teny, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Ushirikishi nchini humo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *