Rais William Ruto amempongeza Rais wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo.
“Tunamtakia Rais Nandi-Ndaitwah, ambaye ni Rais wa tano wa Namibia kila la heri na ufanisi anapochukua jukumu la kuhudumu katika afisi kuu zaidi ya taifa lake,” alisema Rais Ruto.
Kupitia mtandao wa X baada ya kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Nandi-Ndaitwah, Rais Ruto alisema ana imani kwamba Rais huyo mpya atachochea maendeleo na ustawi, kutokana na tajiriba yake katika utumishi wa umma.
“Kutokana na tajiriba yake katika utumishi wa umma, uongozi na ukombozi wa taifa hilo, nina imani kuwa atachochea maendeleo na ustawi wa nchi hiyo,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa Kenya iko tayari kufanya kazi kwa karibu na Rais Nandi-Ndaitwah na serikali ya Namibia, kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.
Ilikuwa ni sherehe maradufu kwa Namibia, huku taifa hilo pia likiadhimisha miaka 35 tangu lipate uhuru.
Viongozi wengine waliohudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Nandi-Ndaitwa kuwa Rais, ni pamoja na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Joao Lourenco wa Angola, Felix Tshisekedi wa DRC, Hakainde Hichilema wa Zambia, Duma Boko wa Bostwana na Daniel Chapo wa Msumbiji, miongoni mwa wengine.